WADAU WA MICHEZO WAPATA ELIMU KUHUSU MATUMIZI YA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU MICHEZONI
service image
31 Oct, 2022

Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la michezo la Taifa (BMT) Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kwa kushirikiana na United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization (UNESCO) imeendaa semina ya siku tatu kwa vyama vya michezo, walimu wa shule mbalimbali na maafisa michezo wa Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam.

Semina hiyo imeanza leo tarehe 31 Oktoba na itahimishwa tarehe 3 Novemba, 2022 ambayo inaendeshwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwa lengo la kutoa elimu juu ya dawa za kuongeza nguvu michezoni.

Akizungumzia semina hiyo Mratibu wa wa Doping Tanzania, Dk. Christine Luambano ambaye pia ni Daktari wa Wizara yenye dhamana ya Michezo alisema wameandaa semina hiyo ambayo itakuwa na mada tofauti kwa siku hizo nne (4) ili kutoa elimu kwa wadau hao ili nao wakatoe mafunzo kwa wanamichezo wao.

"Tumeandaa semina hii ili kuwapa elimu viongozi wa vyama vya michezo, walimu wa shule ambao wanamichezo wanaanzia chini pamoja na maofisa kutoka wilaya za mkoa Dar es Salaam ili kutambua madhara ya kuongeza nguvu katika mashindano, "alisema.

Alisema kuongeza nguvu ina madhara mbalimbali ikiwemo kumkosesha haki mwanamichezo ambaye amefanya mazoezi kwa bidii ili kushinda mashindano.

"Unakuta mchezaji amejiandaa vyema ili kushinda ila unakuta mwingine ametumia dawa za kuongeza nguvu hivyo anashinda kutokana na dawa alizotumia na kudanganya jamii, " alisema.

Upande wa Ofisa wa Michezo wilaya ya Temeke, Ingridy Kimario alisema semina hiyo amejifunza mambo mengi hasa ukitumia dawa ukiwa unaumwa kipindi cha mashindano ukipimwa unaonekana umetumia dawa ya kuongeza nguvu michezoni.

"Leo nimepata elimu kubwa sikufahamu kama baadhi ya dawa zinazotibu mafua ukienda kupimwa unakutwa ametumia dawa za kuongeza nguvu,"alisema.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mchezo wa Kriketi (TCA), Taher Kitisa alisema mafunzo hayo yatasaidia wanamichezo kutambua madhara ya kutumia dawa za kuongeza nguvu.