DOKTA ABBASI ATAKA KAZI NA MATOKEO KATIKA SEKTA YA MICHEZO
service image
15 Sep, 2022

    Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi
amewataka wasaidizi wake kutoka Sekta ya Michezo ikiwemo Idara ya Maendeleo ya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa(BMT) na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kutekeleza kazi zao kwa matokeo makubwa zaidi.

Rai hiyo ameitoa leo Septemba 15, 2022 wakati wa kikao nao ambacho amekiitisha kupata taarifa za utekelezaji wa maagizo tofauti ya Viongozi pamoja na kujua hatua iliyofikiwa katika miradi mbalimbali iliyopo.



"Sekta ya michezo ni sekta muhimu sana kwa Wizara na nchi, kila mtu kwa nafasi yake akaze hasa,"alisema Dkt. Abbasi.

Aidha, Dkt.Abbasi amewataka watendaji wa Idara ya Maendeleo ya Michezo kuwasilisha taarifa ya hatua iliyofikiwa katika miradi 7 ukiwemo wa Uwanja wa Dodoma, 'Sports Arena', Maboresho ya Viwanja vya CCM, Shule 56 za michezo, Sehemu ya mazoezi Uwanja wa Benjamin (GYM), na Matengenezo ya Uwanja wa Benjamin ndani ya siku (7).

Dkt. Abbasi pia, amemtaka Mkuu wa chuo cha Malya Mganga kutangaza kozi kwa wingi ikiwemo kituo za kituo cha Dar es salaam.

"Bado siridhishwi na programu mnazoendesha, mahitaji ni makubwa shirikianeni na wadau wengine,"alisisitiza.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa BMT Neema Msitha, amemtaka kushirikiana na Idara ya Michezo kuhakikisha programu ya Mtaa kwa Mtaa inazinduliwa wakati wa mashindano ya Taifa Cup mwaka huu pamoja na kutoa maelekezo kwa vyama vya michezo na wanamichezo kufuata miongozo na taratibu katika kufanya michezo.