Mhe. Mchengerwa: Napenda nione Mapinduzi ya Maendeleo katika Sekta ya Michezo

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ameitaka Bodi ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kusimamia sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali na kushauri katika maeneo tofauti kwa lengo la kuleta mapinduzi ya kimaendeleo katika sekta ya michezo nchini.
Rai hiyo ameitoa leo Aprili 20, 2022 wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi ya Baraza hilo yenye jukumu la kusimamia taasisi hiyo ya michezo nchini, watakaodumu kwa miaka mitatu kuanzia Aprili,2022 hadi 2025 huku akiwataka kuleta mapinduzi ya kweli katika sekta hiyo.
Wajumbe hao wa bodi wanaongozwa na Mwenyekiti aliyerudi kwa awamu nyingine Leodgar Tenga, Prof. Mtambo Mkumbukwa, Ally Mayai, Tuma Dandi, Yusuph Singo, Ameir Mohamed kutoka Zanzibar na wajumbe watatu watateuliwa hapo baadae.
"Hamkuteuliwa kwa bahati mbaya, nyie ni wabobezi katika shughuli za michezo, sina hofu na tunawapa baraka zote,"alisema Mhe. Mchengerwa na kuongeza kuwa;
"Tutakuwa bega kwa bega katika kuleta mapinduzi ya maendeleo katika sekta hii, mna jukumu la kufuatilia shule zilizotengwa kwa ajili ya michezo, michezo inafundishwa mashuleni pamoja na maendeleo ya miundombinu ya michezo,"alieleza
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka kuimarisha usimamizi wa 5% ya fedha za mfuko wa maendeleo ya michezo unaotokana na mchezo wa kubashiri ili timu za taifa zinufaike na fedha hizo ikiwemo kuboreshewa miundombinu ya michezo, kuongeza uwezo kwa wataalam pamoja na kuendeleza vipaji kwa vijana.
Amewataka kubuni vyanzo vipya vya mapato katika Baraza hilo na kuhakikisha utawala bora unaimarika katika vyama na mashirikisho ya michezo nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Leodeger Tenga, ameeleza kuwa hotuba ya Mhe. Waziri itakuwa mwongozo wao katika kutekeleza majukumu yao, na kumshukuru waziri kwa dhamana aliyowapa huku akimwahidi kuyateleza kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya BMT.