MSITHA ASISITIZA UWAZI NA UWAJIBIKAJI WA VIONGOZI WA VYAMA KWA WADAU WAO.
service image
08 Sep, 2022

          Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amewataka viongozi wa vyama kuzingatia misingi ya Utawala bora ikiwemo kuwa wawazi na kuwajibikaji kwa wanachama na wadau
wao ili kuondoa malalamika yanayojitokeza kwa wadau hao kwa kutokuwa na taarifa za fursa na mambo tofauti yanayoendelea ndani ya baadhi ya vyama vya michezo nchini.



Hayo yameelezwa leo Septemba 07, 2022 na Mtendaji Mkuu huyo wa BMT alipokutana na kufanya kikao na Viongozi wa Juu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ambapo wamezungumza mambo tofauti ya maendeleo ya michezo nchini pamoja na tuhuma mbalimbali zilizowasilishwa katika ofisi za BMT.

"Tuendelea kuboresha yale yanayowezekana ili tuendelee kusukuma gurudumu la maendeleo ya michezo kwa kuwa wawazi, wawajibikaji kwani watu pekee wa kuyafanya haya ni sisi,"alisema na kuendelea kuwa:

"Njia pekee ya kusukuma hili ni pale ambapo kutakuwa na maelewano na na hakuna kelele baina ya nyie Kamati, Mashirikisho na vyama vya michezo na wadau wenu,"alisema Msitha.

Kwa upande wao Viongozi hao wa TOC wameeleza kuwa wamekuwa wakiendesha masuala ya chama kupitia vikao vyao na wanachama ingawa yapo mambo mengine huyafanya kutokana na maelekezo ya kamati yao ya kimataifa (IOC).

Kikao hicho kilimhusisha Katibu Mtendaji wa BMT, Msajili wa vyama vya michezo Riziki Majala, Mkaguzi wa Ndani George Otieno, Afisa Michezo Mkuu Allen Alex pamoja na Watendaji wakuu wa TOC Rashid Gulam Rais, Makamu wake Henry Tandau na Katibu Mkuu Filberth Bayi.