SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO ZAIDI NA SERIKALI YA VENEZUELA KATIKA SEKTA YA MICHEZO.
service image
08 Sep, 2022

           Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu, leo tarehe 06 Septemba, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Afrika kutoka Jamhuri ya watu wa Venezuela Mheshimiwa Yuri Pimentel Moura, kuhusu kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Venezuela katika Sekta ya Michezo.

Akizungumza katika kikao hicho, Yakubu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuwekeza zaidi katika Sekta ya Michezo, hivyo kwa kupata wataalam zaidi kutoka nchini Venezuela kutasaidia kuboresha na kuendelea kuibua vipaji zaidi nchini.

Nayo Serikali ya Venezuela kupitia kwa Mhe. Moura imeeleza kuwa Tanzania na Venezuela ni marafiki wa muda mrefu tangu enzi za Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuahidi kufanyika kwa haraka kikao cha mapema na Uongozi wa Wizara yenye dhamana ya Michezo ili kuainisha maeneo ya kushirikiana katika Sekta ya michezo baina yao na Tanzania.

“Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika Sekta ya michezo kwa kuwa tunaanza kuviendeleza vipaji vya watoto kuanzia ngazi ya chini pamoja na uwepo wa miundombinu ndio maana tumepiga hatua,hivyo ni vyema mapema iwezekanavyo tukawa na mkutano wa moja kwa moja hata kama ni kwa kupitia mtandao, ili tuainishe maeneo ya kushirikiana,”alisema Mhe.Moura.